Tunakupa unachohitaji sasa na baadae

Propellerads
  • WELCOME TO Adonisstunner Blog FOR UPDATED NEWS AND ENTERTAINMENTS

    Search

    Jumamosi, 16 Julai 2016

    YASIKIE HAYA JUU YA PROF.LIPUMBA

    MAMBO 30 YANAYOTHIBITISHA KUWA PROFESA LIPUMBA AMECHANGANYIKIWA, ANACHANGANYWA AU ANAJICHANGANYA?
    Na. Abdallah Yusuph Juma, yabduljuma72@yahoo.com

    15 Julai 2016.

    1.Nikiwa mwanachama (wa zamani) imara wa CUF hapa Marekani nimeendelea kusikitishwa na namna aliyekuwa Mwenyekiti wa chama changu cha zamani cha CUF anavyopelekeshwa. Naamini lipo kundi lenye nia ovu linalommaliza mwenyekiti huyu bila yeye kujua, kundi hilo ovu limemyumbisha sana kiongozi huyu na sasa linamwekea kitanzi akate roho. Nimefanya utafiti wa kutosha kuhusu kadhia na mgogoro wa uongozi ndani ya chama cha CUF na katika maadishi haya naweza kueleza nukta 30 na mambo 30 ambayo wana CUF popote pale walipo wanaweza kuyatafakari, ayah ii ya utangulizi ni jambo la kwanza nililotaka kusema.

    2.Mwaka jana 2015 ni Lipumba huyu huyu ndiye alizinguka nchi nzima akieleza UKAWA utakwenda kushindana na CCM kama BLOCK moja ya vyama vya upinzani. Baadaye kukawa na taarifa atajondoa UKAWA ili chama chake cha CUF kiungane na chama cha ACT cha Zitto Kabwe na Lipumba agombee uenyekiti. Taarifa zikaendelea kuwa Lipumba anabaki katika chama chake lakini akitaka kuwa mgombea urais kupitia UKAWA. Inasemekana chama cha CHADEMA kilikataa mpango huo kwani kulikuwa na makubaliano kuwa chama cha CUF kimetoa mgombea Urais wa Zanzibar, cha CHADEMA kitatoa mgombea urais wa Muungano. Kitendo cha Prof. Lipumba kilionekana kama “kutumika” na wabaya wa vyama vya upinzani, hasa chama cha CCM.

    3.Taarifa zikaendelea kuwa Lipumba amefuatwa na viongozi wa waislamu ili ahakikishe anagombea URAIS kwani ilionekana UKAWA itasimamisha mgombea mkristo na CCM mgombea mkristo pia. Yote haya yalitokea si kwa bahati mbaya, ila ni kwa sababu kuna watu wanamyumbisha msomi huyo. Mimi nilitafakari hali ile na kujiuliza, ikiwa kuna hao viongozi wa kiislamu wanataka mgombea mwislamu asimamishwe na chama cha CUF ili waislamu wamchangue, mbonaa mwaka 2000 Lipumba akiwa mwislamu alipambana na Benjamini Mkapa Mkristo na Mkapa alishinda kwa mbali? Kama waislamu wanaotajwa kumrubuni Lipumba wangekuwa wakweli kwa nini wasingempigia kura za kutosha mwaka huo ili ashinde? Takwimu za CIA zinaonesha kuwa kwa nchi ya Tanzania Waislamu wanafika milioni 25 huku wakristo wakiwa milioni 22 na wasio na dini milioni 3. Kama waislamu milioni 10 wangeamua kukipgia kura chama cha CUF Lipumba angemshinda Mkapa kwa kura nyingi? Kwa hiyo hao waislamu waliomdanganya Lipumba mwaka jana na wanaoendelea kumdanganya mwaka huu labda ni wale wa BAKWATA ambao wote ni CCM, kwa hiyo Lipumba anaweza kuwa anadanganywa na CCM kupitia waislamu wa BAKWATA na wala siyo waislamu safi wanaojiheshimu na kumtukuza Allah wa mbinguni ambao wengi wao wameteswa mno na madhila na dhuluma za BAKWATA!

    4.Baadaye taarifa zikazidi kuwa Lipumba anajipanga kuchukua fomu ya uenyekiti kupitia chama cha CUF lakini baadaye akazidiwa kete na Katibu Mkuu wake, Seif Hamad, ambaye, Seif pamoja na viongozi wengi wa Bara na Zanzibar wa chama hicho walikataa mpango wa Lipumba kwa msisitizo wa kukiachia CHADEMA mamlaka ya kumtafuta mgombea urais. Edward Lowassa alipokimbia CCM na kutua CHADEMA michakato yote kuanzia kumpokea, kumsifia na kumsafisha – ilifanywa na Lipumba mwenyewe, akiwa Mwenyekiti kiongozi wa UKAWA. Hata PRESS CONFERENCE ya kumkabirisha Lowassa ilifanywa kwenye ofisi za chama cha CUF makao makuu Dar na msemaji mkuu alikuwa ni Lipumba?

    5.Baada ya Lowassa kutangazwa kuwa mgombea tulisikia sarakasi zinaanza na Lipumba anataka kutoka chama cha CUF akiwa na makada wa chama hicho wakiwemo wabunge na wakurugenzi wake. Maalim Seif Sharif wa Zanzibar na wenzake wakazuia mipango hiyo halafu tukasikia Lipumba anajiuzulu. Kwanza alikwenda makao makuu ya chama chake kujiuzulu wanachama wakamkataza, ndipo alikwenda kwenye hoteli moja ya huko Dar Es Salaam na kujiuzulu akitoa sababu kadhaa. Lipumba alipojiuzulu alisema “NAFSI YAKE IMEMSUTA” katika kile kilichotajwa kama “kuja kwa Lowassa kwenye umoja wa UKAWA”. Sababu nyingine ya Lipumba kujiuzulu ilikuwa ni “kujiondoa ili asiwe kizuizi na kikwazo cha chama chake ambacho ni kama kilikuwa kinamtuhumu kuwa anakizuia kufanya maamuzi muhimu”.
    Sijui nini kilimkuta msomi huyu nguli ambaye anaheshimika kitaifa na kimataifa. Kuondoka kwa Lipumba CUF kuliacha pengo kubwa la kiuongozini wa chama cha CUF.

    6.Chama cha CUF kilikosa kabisa kiongozi maalum kwenye kukubaliana majimbo ambapo CHADEMA ilimpeleka Mbowe, NCCR ikampeleka Mbatia, CUF ilimpeleka Ofisa aitwaye Lugone na Paku bila kumsahau Ndugu Shaweji Kkeketo ambaye ni msimamizi wa uchaguzi wa chama hicho – hawa ni vijana wadogo kabisa kushindana na kina Mbowe, Lowassa na Mbatia kwenye vikao! Kundoka kwa Lipumba ambaye alikuwa anawamudu kina Mbowe, Mbatia na Lowassa kulikuwa kitendo cha makusudi cha kuifanya CUF ikose uongozi na imezwe na vyama hivyo ambavyo huwezi kuviamini sana. Tulishuhudia CUF ikiyumba na chama cha CHADEMA kikisimamisha wagombea kwenye majimbo mengi sana ambayo yalikuwa ni ya chama cha CUF na bila kupata mtu wa kukikanya chama cha CHADEMA. Huu ni wakati ambapo Maalim Seif alikuwa anashindana kuchukua ushindi Zanzibar na asingeweza kufanya yote mawili. Lipumba alikiacha CUF kikiwa yatima na isiyo na mbele wala nyuma NA kitendo chake ni sawa na “mama aliyebeba mimba kwa miezi sita akapitia mateso yote makubwa, akajifungua kwa uchungu na kisha kwa makusudi akaenda kukitupa kichanga chake chooni kiliwe na funza”.

    7.Chama cha CUF kilikosa kiongozi shupavu wa kuvutia kura nyingi kutoka kwa wapiga kura. Baada ya Lipumba kujiuzulu aliamua kukaa pembeni, alisikika mara kadhaa akisema anajielekeza kwenye tafiti mbalimbali ili baada ya uchaguzi mkuu aisadie serikali ijayo katika masuala ya kiuchumi. Alisimama wazi kabisa kumpinga mgombea wa UKAWA, Edward Lowassa, bila kujali kuwa kumpinga Lowassa kulikuwa na maana ya kuathiri kura za wabunge na madiwani wa chama chake mwenyewe cha CUF. Maana, Lowassa na Duni Haji ndiyo walibeba bendera ya UKAWA, kumpinga Lowassa alikokuwa anafanya Lipumba kwenye vyombo vya habari wakati wa Uchaguzi Mkuu kulikuwa na maana ya kwamba wananchi wasiunge mkono mabadiliko na kwa minajili hiyo hata chama chake cha CUF kingelipaswa kuathirika na msimamo wake na kingeweza kukosa wabunge na madiwani wengi kwa sababu aliwaonesha wananchi ya kwamba mabadiliko yameingiliwa na bundi na ni bora yale ya CCM kuliko haya ya UKAWA.

    8.Lipumba lionekana akiwa Rwanda na mmoja wa vijana Maarufu wa Usalama wa Taifa (TISS) wakinywa JUISI na alipelekwa na Usalama wa Taifa kutembelea wizara mbalimbali za Rwanda, akijiandaa kusaidia serikali ijayo, jambo ambalo alikuwa amelieleza kwenye barua yake ya kujiuzulu (Rejea Kumbukumbu ya Barua hiyo). Zipo taarifa kuwa mkakati wa kwenda Rwanda ulipendekezwa na Rais Magufuli mwenyewe na zipo taarifa kuwa Magufuli na Lipumba walikuwa wanafanya vikao vingi aliporudi kutoka Rwanda na hata VIDEO CONFERENCE kila Magufuli alipokuwa kwenye kampeni. Ndiyo maana leo ukiuliza Lipumba alishiriki kwenye kampeni ipi kusaidia wagombea wa chama cha CUF washinde mwaka jana, utagundua hakufika kokote. Huo ulikuwa ni mkakati maalum wa kuhakikisha CUF kinashindwa vibaya katika uchaguzi ili LIPUMBA na timu yake wasujudiwe kwa ukuu wa wao kuona mbali na kutaka kujitoa kwenye umoja wa UKAWA.

    9.Kuondoka kwa Lipumba kulikiparaganyisha chama cha CUF na wakurugenzi wake waligawanyika. Taarifa za wazi kutoka CUF zinaonesha kuwa Abdul Kambaya wa idara ya habari, Abdallah Mtolea wa kitengo cha mambo ya nje ya nchi ya chama hicho ambaye ni mbunge wa Temeke sasa, Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge wa Kaliua hivi sasa (wakati huo akiwa Katibu Msaidizi wa Maalim Seif na Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha CUF) na Mbunge Mstaafu Kuruthum Mchuchuri (Viti Maalum wakati huo na kwenye uchaguzi akigombea jimbo la Rufiji Pwani + Mkuu wa Idara ya Haki za Binadamu na Uenezi) walikuwa ni viongozi ambao walisimama nyuma ya Lipumba kwa udi na Uvumba na waliapa kuwa kama atatoka kwenye chama cha CUF na kwenda chama cha ACT cha Zitto Kabwe wangemfuata huko. Bahati mbaya Lipumba hakuondoka CUF wakati ule, alibaki kuwa mwanachama na viongozi hawa wote wakaenda majimboni kugombea ubunge isipokuwa Abdul Kambaya ambaye alikuwa na jukumu la kusaidia Kampeni kwa mujibu wa kazi za idara yake ya habari na mahusinao na umma alipewa fedha za kwenda kwenye kampeni shilingi milioni 3 na hakwenda kwenye vituo kwa ajili hiyo na badala yake alibaki Dar Es Salaam akishiriki kampeni katika baadhi ya kata na fedha zile hadi leo Kambaya hajazirejesha. Hata alipokwenda kumnadi mgombea ubunge wa Kinondoni Saidi Mtulia (mbunge wa sasa kupitia chama cha CUF), Kambaya alimfanyia rafu za wazi mbunge huyo kijana ambaye pia alimshinda Kambaya kwenye kura za maoni ndani ya chama cha CUF katika kuwania jimbo hilo hilo.

    10.Wakurugenzi walokuwa wakitaka UKAWA ivunjike, walipokwenda majimboni, baadhi yao walipata ushindi mzuri. Mfano ni Magdalena Sakaya ambaye, pamoja na kutoamini na kutotaka umoja wa UKAWA uwepo alishindana kule Kaliua na kumshinda Kapuya wa chama cha CCM. Wanachama wa chama cha CUF kutoka mkoa wa Tabora wameeleza kuwa kama CHADEMA wangesimamisha mgombea kwenye jimbo la Magdalena Sakaya, kiongozi huyo angepata nafasi ya nyuma ya CHADEMA na Kapuya angeshinda. Nguvu zilizompa Sakaya jimbo la Kaliua zilitokana na ushirikiano wa UKAWA. CUF peke yake isingeweza. Hata jimbo la Temeke la Abdallah Mtolea, kama kusingekuwa na UKAWA jimbo hilo lingechukuliwa kirahisi na CCM na hali ya siasa ilivyokuwa mgombea wa chama cha CUF angeshika nafasi ya tatu nyuma ya CHADEMA

    11.CUF iliyakosa majimbo ya Pangani - Tanga, Rufiji - Pwani, Mkinga – Tanga, Segerea – Dar Es Salaam, Mbagala – Dar Es Salaam, Kisarawe – Pwani, Ruangwa – Lindi, Mtama – Lindi, Lindi Mjini – Lindi, Nachingwea – Lindi, Namtumbo – Ruvuma, Tunduru Kaskazini na Tunduru Kusini – Ruvuma na majimbo mengine mengi. Kwa hiyo, kama Lipumba angekuwa na msimamo akabakia CUF na kuongeza nguvu kwa wabunge wake ni dhahiri chama cha CUF kingekuwa na wabunge 15 wa ziada ambao wangefanya idadi ya wabunge wa kuchaguliwa chama hicho kwa Tanzania Bara kufika 25 na idadi hiyo ingeongeza kura ambazo zingeongeza wabunge wa Viti Maalum upande wa bara kufikia wanane hadi kumi tofauti na watano wa sasa. Kukosekana kwa Lipumba katika chama chake mwaka jana ni sawa na mzazi aliyeamua kumuacha mtoto wake wa miaka 2 hadi 4 kukatiza kwenye barabara kuu ya mabasi yaendayo kasi hapo Tanzania au huku Marekani akiwa yeye mwenyewe. Uamuzi wa Lipumba ulikuwa ni “adhabu ya kujiua” kwa chama cha CUF. Kwa hiyo CCM ilisheherea ushindi mnono kwenye majimbo yote niliyoyataja hapo juu kwa sababu Lipumba alisaliti chama cha CUF na kupunguza nguvu ya ushindi na baadhi ya watu ndani ya chama cha CUF wanaamini lengo la Lipumba lilikuwa ni kuisaidia CCM.

    12.Mwaka 2015 haikuwa mara ya kwanza kwa Lipumba kuisaidia CCM kwenye uchaguzi. Yeye mwenyewe amewahi kutamka kuwa mwaka 2010 viongozi wa dini ya kiislamu walimfuata kumuomba atoe usaidizi ili Jakaya Kikwete wa CCM apate ushindi. Viongozi hao waliomfuata Lipumba ni wa BAKWATA ambao wanafahamika vizuri kwa misimamo yao ya kuitetea na kuilinda CCM. Haya siyo maneno yangu, ni maneno ya Lipumba mwenyewe akiwa kwenye msikiti mmoja huko Dar ES Salaam na mtu yeyote anaweza kubonyeza kiunganishi kwenye YOUTUBE kumsikiliza Lipumba huyu huyu wa chama cha CUF akieleza alivyosaidia ushindi wa Kikwete mwaka 2010 ilihali chama chake kikianguka vibaya na yeye akiwa ni mgombea. Kwa waislamu safi na wanaofuata dini yao vizuri, kiongozi anayetumika na kundi la BAKWATA iliyobeba CCM hawezi hata siku moja kujisifu kuwa alikuwa anasimamia maslahi ya waislamu, tena kwenye nchi ambayo ina idadi inayokaribiana kati ya waislamu na wakristo, idadi inayomaanisha kuwa ili chama cha siasa kipate ushindi kwenye uchaguzi ni lazima kiungwe mkono na dini zote kuu katika nchi.

    13.Mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na Magufuli Pombe wa CCM kushinda urais na huko Zanzibar Maalim Seif kunyang’anywa ushindi wa chama cha CUF, wakati chama cha CUF kikiendesha kampeni ya kumshinikiza Kikwete na baadaye kumshinikiza Magufuli ili watatue dhuluma ya Zanzibar. Vyombo vya habari vilimuonesha Lipumba akiwa Ikulu, akimtembelea Magufuli na kumpongeza kwa ushindi mkubwa na kumhakikishia anamuunga mkono. Wakati chama cha CUF kinamsusa Magufuli na Shein katika bunge, Lipumba anakwenda ikulu kumpongeza Magufuli kwa ushindi mnono na kwa kutochukua hatua kuokoa ushindi wa Maalim Seif kule Zanzibar. Nilipoona hali ile nikajua Lipumba amemalizika. Taarifa za ndani za ikulu zinaonesha Lipumba alikwenda kupeleka mrejesho wa tafiti zake za kiuchumi za namna Rwanda inavyoweza kusaidiana na Tanzania katika maeneo ya kiuchumi. Kitendo cha Lipumba kumtembelea na kumpongeza Magufuli kilifanywa pia na Dk. Slaa wa chama cha CHADEMA lakini yeye akimpongeza Magufuli kupitia gazeti la Raia Mwema na Raia Tanzania.

    14.Taarifa za ndani zinaonesha kuwa Lipumba kupitia kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa NSSF (ambaye ni Rafiki Mkubwa wa Lipumba) ndugu Ramadhani Dau, alikuwa ameahidiwa nafasi muhimu na kubwa sana ndani ya serikali ya Magufuli. Kwa bahati mbaya Magufuli hakumtegemea Dau kwenye serikali yake mpya, akamuondoa kutoka NSSF na kukata mizizi na ushawishi wake serikalini. Kuondolewa kwa Dau serikalini ndiko kulivunja mikakati yote ya Lipumba kuitumikia serikali ya JPM kwenye sekta ya uchumi kama alivyokuwa ameahidiwa. Huku serikalini maafisa wa ngazi za juu wa TISS wakaulizana, nani ataweza kumdhibiti Lipumba kama Dau hayupo? Jibu likawa ni HAYUPO. Rais Magufuli akakubaliana na TISS kuwa Lipumba siyo ASSET tena kwenye serikali yake na kazi ya kumpiga danadana ya utekelezaji wa ahadi ya kupewa wadhifa serikalini ikaanza na kukomaa.

    15.Siku chache baada ya Lipumba kugundua kuwa Magfuli hamhitaji tena, mwenyekiti huyo alianza kujitokeza hadharani kulipiza kisasi cha kusalitiwa na Dau na Magufuli kwa kumpinga Magufuli akieleza serikali ya Magufuli isivyochukua hatua za kiuchumi na inavyominya demokrasia. Lipumba huyu ni yule yule ambaye alikimbilia Ikulu kumpongeza Magufuli na kumuunga mkono na akatangaza hadharani kumuunga mkono. Baada ya kukosa ule wadhifa aloahidiwa akageuka kuanza kumponda swahiba wake. Na hii siyo mara ya kwanza, Lipumba huyuhuyu ndiye aliyemsaidia Kikwete kushinda urais mwaka 2010 kwa kudanganywa na BAKWATA ya CCM na ni Lipumba huyohuyo ndiye alikuwa akizunguka huku na kule kuponda uwezo wa Kikwete katika kuongoza nchi baada ya yeye mwenyewe kushiriki kumnusuru asikose madaraka mwaka 2010. Ni Lipumba huyo huyo ndiye alikuwa mstari wa mbele kumkaribisha Lowassa kwenye UKAWA na kumsafisha mbele ya vyombo vya habari na Lipumba huyohuyo ndiye aliyejiuzulu uenyekiti wa chama cha CUF kwa sababu ya ujio wa Lowassa. Ni Lipumba huohuyo ndiye baada ya mwaka mzima anajaribu kurudi kwenye wadhifa wake – kwa wanaomfahamu hajawahi kuwa mwanasiasa mwenye msimamo, ni mtu wa kuyumba njia nzima, ni mtu wa kusikiliza kila analoambiwa hata na watu aliowazidi akili na utashi mara 1000.

    16.Wakati haya yote yakiendelea;

    A. Kundi lile lile la mwaka 2015 lililotaka kung’oka na Lipumba kutoka chama cha CUF liliendelea na harakati zake hasa kule kwenye jiji la Dar Es Salaam. Kundi hilo likiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama cha CUF, BI. Magdalena Sakaya, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho kutoka Zanzibar ndugu Yusuph (Mbunge), wajumbe wa Halmashauti Kuu ya Barzza Kuu la chama cha CUF ambao ni Thomas Malima wa Kigoma, Ashura Mustapha wa Dar Es Salaam, Abdul Kambaya wa Dar Es Salaam, Abdallah Mtolea wa Dar Es Salaam, Ndugu Kaswaka wa Dar Es Salaam, Ndugu Masud wa Handeni, Ndugu Mchuchuli wa Rufiji, Ndugu Shashu Lugeye wa Shinyanga, ndugu Kapasha wa Tabora na baadhi ya maafisa wachache wa chama cha CUF wakaanza kusuka mkakati wa kumuwezesha Lipumba kurudi kwenye nafasi yake ndani ya chama cha CUF.

    B. Malengo mahsusi ya kundi hili ni kulinda nyahdifa zao. Kwa mfano, Magdalena Sakaya amekuwa na hofu ya kuipoteza nafasi yake ya Unaibu Katibu Mkuu baada ya kubaini kuwa hujuma alizokifanyia chama cha CUF kwa kushirikiana na wenzake toka mwaka 2015 kwa kupinga UKAWA na kumrubuni Lipumba waondoke chama cha CUF na kwenda chama cha ACT yeye na wenzake – zinamuweka mahali pabaya katika siasa za kudumu ndani ya chama cha CUF. Wakurugenzi wa chama hicho kama Abdul Kambaya pia wana hofu hizo hizo. Wote hawa wamekuwa wakiamini kuwa nyadhifa zao za uongozi ndani ya CUF zitakuwa za uhakika tu pindi Lipumba akiendelea kuwa Mwenyekiti. Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama cha CUF akiwemo Bibi Ashura Mustapha wanaamini kuwa uwepo wa Lipumba ndiyo unaweza kuwapatia nafasi za Viti Maalum. Mara kwa mara Bibi. Ashura amekuwa akinukuliwa na wanachama wa chama cha CUF akilaani kuwa alinyimwa Ubunge wa viti maalum mwaka jana kwa sababu tu Lipumba hakuwepo. Lawama hizo pia zinatolewa na Mjumbe wa KamatI Kuu ya Halmashauri Kuu Bibi Kuruthum Mchuchuli. Katika kuelekea siasa za 2020 kundi lote hili linatafuta wapi litaegemeza mikono yao ili kubaki salama kisiasa.

    17.Kundi hili lilianzisha harakati zake na kufanya makongamano kadhaa ambayo yalishindwa vibaya na hayakuwa na matumaini, wilaya walizozifikia ni pamoja na Kinondoni, Morogoro Mjini, Kaliua, Handeni na Kisarawe. Huko waliwarubuni wanachama wa chama cha CUF kuwa bila Lipumba chama hicho kitakufa na walikwenda mbali kuwaaminisha kuwa mafanikio ya chama cha CUF kwenye uchaguzi wa 2015 yaliletwa na Lipumba na siyo mtu mwingine. Hoja yao ni kuwa chama cha CUF kimepata wabunge wengi kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara na aliyejenga chama kwenye mikoa hiyo ni Lipumba. Swali dogo sana ambalo kundi hili la wanaojiita “wafia chama” limeshindwa kulijibu ni “iweje katika miaka karibia 20 ya uenyekiti wa Lipumba chama cha CUF kilishindwa kupata wabunge angalao watatu Tanzania Bara lakini ulipokuja UKAWA ndio kwa mara ya kwanza chama hicho kikapata wabunge 15 Tanzania bara?”

    18.Harakati za kundi la wanaojiita “wafia chama” ziliendelea kwa kukodi kumbi na kuwalipa fedha wanachama idadi fulani ili washiriki mijadala ya kumhitaji Lipumba. Lilichukua vyombo vya habari na kuvitumia kwenye mijadala hiyo ambayo ilikuwa na mahitimisho ya “Lipumba lazima ARUDI kwenye chama cha CUF”. Lipumba alikuwa anapelekewa mirejesho yote hatua kwa hatua na kwa sababu tayari dili la yeye kupata kazi katika serikali ya Magufuli lilishindikana ikambidi naye aanze kuvutiwa na wazo la kurejea kwenye uenyekiti wake kwa kutumia kisingizio cha kuwa, wanachama wanamhitaji. Kundi hilo likaongozwa pia na Katibu wa CUF wilaya ya Kinondoni ndugu Mkandu na Lipumba akaitishiwa mkutano wa hadhara kata ya Mwananyamala ukipigiwa chapuo na Abdul Kambaya na fedha za mkutano zikichangwa na baadhi ya wabunge wanaounga mkono Lipumba kurejea kwenye chama cha CUF.

    19.Wakati kundi hilo likiendelea na mikakati ya kutaka Lipumba arudi ili linusurike ndipo;

    A.Chama cha CUF kilikutana huko Zanzibar katika kikao cha Barzza Kuu la Halmashauri Kuu ili kupanga tarehe ya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti na Makamo Mwenyekiti. Kwenye kikao hicho kundi la “wafia chama” likiongozwa na Ashura Mustapha, Thomas Malima na Masud kutoka Handeni ndipo walisimama kudai kuwa lazima barua ya kujiuzulu kwa Lipumba ijadiliwe na Mkutano Mkuu kwanza. Wanasheria wa chama hicho Ndugu Abubakar, Ndugu Taslima na ndugu Hashim walitoa ufafanuzi wa kikatiba na kisheria na kuwaelewesha wajumbe hao kuwa ni lazima chama kiende kwenye uchaguzi, wajumbe hao walishikilia msimamo wao na kwa bahati mbaya idadi yao ilikuwa chini ya 10 miongoni mwa wajumbe 70 wa Halmshauri ya Juu ya chama cha CUF. Kwa hivyo maamuzi yakafikiwa kuwa chama cha CUF kitaitisha mkutano mkuu kuchagua mwenyekiti mpya na makamo mwenyekiti mpya.

    B.Kuona hivyo kundi la wanaojiita “wafia chama” likakimbia kwa Lipumba kumjulisha kuwa lazima achukue maamuzi ya haraka ya kutangaza kurejea kwenye uenyekiti aliojiuzulu ili mambo anuai yatokee ikiwemo chama cha CUF kupata mpasuko au kulifanya Baraza Kuu la Halmashauri Kuu likutane tena kujadili mamo yanavyokwenda na ikiwezekana Baraza hilio lisitishe kuitisha mkutano mkuu wa chama cha CUF kwa kuhofia kuwa kufanya hivyo kutakuwa ni kukivunja CUF. Mipango ikasukwa haraka haraka na mwanasheria mmoja (jina linahifadhiwa) akatumika kuandika kilichoitwa barua ya Lipumba kurudi kwenye wadhifa wake, Lipumba akaikabidhi kwa Maalim Seif katibu Mkuu wa chama cha CUF.

    20.Taarifa za ndani ya chama cha CUF zinaonesha kuwa Maalim Seif alimjibu Lipumba kwa barua akimjulisha chama hicho kinawaachia jambo hilo wanasheria wake na vikao vya juu vya CUF. Barua ambayo Seif alimuandikia Lipumba ilimueleza kuwa Mwenyekti huyo wa Zamani akae mbali na masuala ya chama hadi hapo jambo hilo litakapoamuriwa na vikao vya chama. Seif akajisafiria kuja ughaibuni kuhangaikia ushindi wake alioporwa na Shein. Akiwa huku nje taarifa zinaonesha kuwa Abdul Kambaya na Magdalena Sakaya wakaitisha vyombo vya habari na kumtaka Lipumba awe muongeaji wa masuala ya bajeti, lakini wakamtaka aweke hadharani mbele ya vyombo vya habari, barua yake kwa Katibu Mkuu kuwa anarejea katika wadhifa wake. Aliyetoa fedha kwa ajili ya kuita vyombo vya habari ni Magdalena Sakaya, tena akifanya hivyo baada ya Mkurugenzi wa Fedha wa chama cha CUF, Ndugu Joran Bashange kukataa kutoa fedha za vyombo vya habari. Taarifa za ndani za chama cha CUF zinasema Abdul Kambaya alipokea pia kiasi cha fedha kutoka kwa Magdalena Sakaya na ndizo zikatumika pia kukodishia mabasi mawili yaliyochukua wanachama wa kundi linalojiita “wafia chama” kutoka kata za Tandale, Manzese na kata ya Ukanda wa Gaza ambao walipelekwa makao makuu ya CUF Dar Es Salaam. Wanachama hao walipewa posho za ziada, fedha za kuchora mabango na tisheti ambazo zilichapishwa kwa udhamini wa Mkurugenzi wa Ulinzi wa chama hicho ambaye ni mbunge kutoka Pemba ndugu Yusuph.

    21.Siku ya siku ndipo Lipumba akatangaza kuwa anarejea kwenye wadhifa wake, akitoa tangazo hilo mbele ya vyombo vya habari hivyo kwenye ukumbi wa CUF makao makuu. Nje ya ukumbi, kundi la wanachama kati ya 30 – 50 waliokuwa wamekodishwa na kupewa mabango na matisheti wakishangilia kwa nguvu zote. Tisheti hizo zilisomeka “Lipumba kwanza Chama baadaye”. Nilipoziaona mitandaoni nikahisi kuwa chama cha CUF kinaelekea kuzimu. Iweje hawa wanaojiita wafia chama na wakiongozwa na wabunge na wakurugenzi na viongozi wa chama hicho hicho waanze kuaminishana kuwa Lipumba ni muhimu kwa chama cha CUF kuliko CUF chenyewe? Iweje watu hawa waamini kuwa ni bora CUF kife lakini Lipumba arudi? Iweje watu hawa waamini kuwa bila Lipumba CUF hakipo na wakati huohuo wakisahau kuwa ni mwaka jana tu mtu huyohuyo aliwasaliti na si mara ya kwanza kufanya hivyo, amewasaliti tangu enzi za Kikwete 2010, akawasaliti kwa kukimbilia kwa Magufuli kujikomba na kumuunga mkono mwaka huu huu 2016 na sasa anaendelea na kutaka kurudi kuwa Mwenyekiti?

    22.Tangazo la Lipumba kurejea kwenye wadhifa wake lilipingwa san asana na vyombo vya habari vyenyewe vikiliripoti kwa shingo upande. Kada wa chama cha CUF ndugu Julius Mtatiro ambaye pia atagombea uenyekiti wa CUF alikuwa wa kwanza katika kurasa zake za mitandaoni “kuponda uamuzi huo wa Lipumba”, alifuatia Maalim Seif akiwa Marekani akieleza kushangazwa kwake na hatua ya Mwenyekiti wake wa zamani na mwisho ile Kamati ya Uongozi iliyoundwa na Halmashauri Kuu la Barzza Kuu la CUF ikatoa taarifa yake ikiongozwa na Twaha Taslima (Mbunge wa Afrika Mashariki na mtu anayetajwa kwa tetesi kuwa anaweza aidha kugombea wadhifa huo au kuendelea kuwa Mwenyekiti), Bi. Saverin Mwijege, Ndugu Abubakari Hamis na wengine – taarifa ya kamati ya chama cha CUF ilieleza bayana kuwa Lipumba hana nafasi tena ya uongozi wa juu kwenye chama cha CUF.

    23.Taarifa zote tatu ambazo naweza kuzichukulia kama zilizopewa uzito na vyommbo vya habari vya Tanzania zilipondwa kwa nguvu na kundi linalojiita la “wafia chama”. Kundi hilo likiongozwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Barzza kuu la CUF lilipiga kambi mitandaoni kutoa taarifa nyingi za kuwashambulia wale viongozi waliotoa taarifa za kupinga kurudi kwa Lipumba. Uchunguzi wa ndani ya chama cha CUF umebaini kuwa sehemu kubwa ya wafuasi wa kundi lijiitalo “wafia chama” ni waliokuwa wanachama wa CUF na wakakihama cham hicho wakati wa kadhia ya Hamad Rashid na CUF (wakahamia ADC) na wengine walihamia ACT Wazalendo mwaka jana (akiwemo mtukanaji maarufu mitandaoni anayejiita “DAVID MAPHONE”.

    24.Uchunguzi unaonesha kuwa huyo David Maphone aliwahi kuwa Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya chama cha CUF wilaya ya Kinondoni kabla hajaondolewa na baadaye kukimbilia ACT. Majina yake halisi ni BAKARI WAYANDA na akaunti feki yake nyingine mitandaoni inatumia majina ya”BAKARI NZINAMO”, na nyingine inatumia majina “TADEI OLE MUSHI”.
    a)Mtukanaji mwingine mwandamizi wa kikundi hicho ni ndugu Milanzi ambaye ana akaunti feki kadhaa za matusi kwa viongozi wa chama cha CUF, moja inatumia majina ya “MILANZI MILANZI MILANZI”, nyingine inatumia majina ya “LIGHTNESS SHIRIMA”.
    b)Mtukanaji wa tatu wa kikundi hicho anaitwa Mohamed lakini kwenye mitandao anatumia akaunti feki zenye majina ya “MPURUTI MWAI” na “KUNTA KINTE”.
    c)Mtukanaji mwingine ni “HUSSEIN MCHOMOLO” ambaye akaunti feki yake inatumia majina ya “HUSSEIN SEIF”.
    d)Mtukanaji mwingine aliyekubuhu na ambaye anatumiwa sana na kundi hili ni Ndugu Kundambanda, msanii wa vichekesho na mwanachama wa CUF aliyegombea ubunge jimbo la Masasi, huyu Kundambanda akaunti feki yake inatumia majina ya “GIDAMANGA DACHI”.
    e)Watukanaji hawa wanatukana viongozi wa chama cha CUF na kuwashushia tuhuma nyingi za kutunga na kila wanachokieleza ni cha uongo, ndiyo maana ukisoma maandiko yao unashuhudia yalivyojaa matusi, hasira, kukata tama, uongo, uzandiki na upuuzi usio na ushahidi wowote. Ndiyo maana inawalazimu wafiche majina yao na kutumia akaunti zisizo za kwao.

    25.Baada ya Maalim Seif na Kamati ya Uongozi kuonesha mwelekeo kuwa Lipumba hana nafasi ya uongozi ndani ya CUF, na kwa kuzingatia kuwa chama cha CUF kimekuwa na msimamo wa kuendelea kuelekea kwenye Mkutano Mkuu wa kuchagua viongozi; kundi hilo la wanaojiita “wafia chama” linaloongozwa na kufadhiliwa na Naibu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya na Wakurugenzi, Mtolea (Temeke), Yusuph (Ulinzi – Zanzibar) na Abdul Kambaya (Kinondoni) limeendelea kufanya vikao vyake katika maeneo ya Dar Es Salaam na kwa sasa limeshapungukiwa na hatua za kuchagua;
    A.Kwanza linafikiria kwa sasa litafute mbinu za kuuzuia Mkutano Mkuu wa chama cha CUF katika Mahakama Kuu ya Tanzania, lengo la kuzuia mkutano huo ni kupata uungwaji mkono wa vyombo vya dola na Chama Cha Mapinduzi ili chama cha CUF kisichague viongozi na kikae kwenye mgogoro kwa muda mrefu na kidhoofike. Kwa mujibu wa mipango ya kundi hili, wakifanikiwa kuzuia mkutano mkuu na kesi ya msingi ikaendeshwa mahakamani muda mrefu itasaidia sana chama cha CUF kupoteza wabunge wengi na madiwani wengi mwaka 2020 na kwa hiyo matamanio yao kukiona CUF kikianguka kwa sababu Lipumba hayupo, yatimie.
    B.Pili, kundi hilo kwa sasa linahaha kutafuta mbinu ya kumchukulia fomu Profesa Lipumba ili awe mmoja wa wagombea. Linafanya hivi likiamini kuwa wagombea Uenyekiti wa chama cha CUF wenye nguvu ni Mtatiro, Taslima na Kuchauka na kundi hilo linaamini kuwa kati ya hao wote hakuna atakayemshinda Lipumba ikiwa kura zitapigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu. Kwa hiyo limeamua kuchukua njia hii ya pili na kwenda nayo sambamba na ile ya kwanza hapo juu kuona ipi itafanikiwa kirahisi.

    C.Tatu, kundi hilo limeanza maandalizi ya kutafuta vijana wahuni, mabaunsa na kikundi maarufu cha “Panya Road” ili kujiandaa kufanya vurugu kubwa siku ya Mkutano Mkuu wa CUF. Katika moja ya mjadala wa kundi hilo Magdalena Sakaya aliwasilisha hoja kuwa Mkutano Mkuu wa chama cha CUF utafanyikia katika hoteli ya Landmark Ubungo kama ilivyotangazwa na Bwana Shaweji Mketo wa Usimamizi wa mambo ya Uchaguzi ya chama cha CUF. Inaonesha kuwa itakuwa rahisi sana kuendesha vurugu katika Ukumbi kama Landmark au Lamada na tayari kundi hilo limeanza kufurahia ikiwa chama CUF kitafanyia mkutano wake mahali hapo. Mpango wa vurugu uliopo ni kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu watakaokuwa wamepewa fedha kusimama na kutaka Lipumba ajadiliwe na kurejeshwa. Kundi hilo linajua kuwa ajenda hiyo itakataliwa na mwenyekiti wa kikao hicho, ndipo wajumbe hao wachache watachukua viti, chupa na mawe yatakayokuwa kwenye mifuko yao na kuanza kuwarushia viongozi wa meza kuu. Vurugu ikiwa kubwa ndani na taharuki kuzidi ndipo mabaunsa, wahuni na vijana wa Panya Road wataingia kwa nguvu na kuendeleza vurugu kubwa hadi mkutano uvunjike kabisa.

    26.Kitendawili ambacho kinasubiriwa na wengi ni Je, Halmashauri Kuu ya Barzza Kuu ya CUF itaruhusu Lipumba apewe fomu na agombee Uenyekiti tena? Vipi kuhusu gharama za kuitisha mkutano huo zifikazo Bilioni 1 Shilingi za Tanzania? Kwa nini chama cha CUF kiamue kuharibu Bilioni 1 Shilingi za Tanzania kwa ajili ya kumrudishia Lipumba uenyekiti wake? Kuna ufisadi kama huo kenye chama cha siasa tena cha upinzani? Wakati huo huo watu wanazidi kuhoji iweje mtu aliyekisaliti chama hicho wakati mgumu kabisa wa mapambano ajaribu kurudi kwa mlango wa nyuma au wa mbele na kupokelewa? Inazidi kuhojiwa pia, sababu zilizomuondoa zimeondoka? Kama nafsi ilimsuta baada ya “kumpokea Fisadi Lowassa” je Fisadi huyo ameshaondoka kwenye huo UKAWA au bado yupo? Na kama Fisadi Lowassa yupo, yeye Lipumba atawezaje tena kufanya kazi na mtu aliyemfanya aondoke wakati muhimu wa mapambano? Lakinii inaendelea kuhojiwa, ikiwa Lipumba hakutaka Lowassa awe mgombea Urais na bado yeye ndiye akampokea, kumnadi na kumtangaza kisha akajiuzulu – Vipi 2020? CHADEMA kikipewa kusimamisha mgombea wa Urais na kikamuweka Lowassa kwa mara nyingine, Lipumba hatasutwa na nafsi kama 2015?

    27.Inaendelea kuhojiwa kuhusu sababu za ndani ya chama chake cha CUF, wakati Lipumba anajiuzulu alidai “anaonekana amekuwa kikwazo ndani ya chama chake” na taarifa za ndani zinanesha alipishana kimtizamo na kimsimamo na Maalim Seif hasa kwenye suala la CUF kuendelea na UKAWA au kutoka. Lipumba alikuwa anataka CUF kijitoe na Maalim Seif akiweka msimamo CUF kibaki. Je, sababu hizo za ndani za kuonekana yeye ni Kikwazo (Lipumba) zimekwishaondoka? Haoni kuwa kurudi kwake katika uongozi ni kuja kuamsha vita mpya na kupelekea CUF kugawanwa kama mbao kama inavyoelezwa na viongozi, wafadhili na wafuasi wa kundi linalojiita ‘wafia chama” ambalo Lipumba mwenyewe amelibariki na mara kwa mara linafanyia vikao nyumbani kwake Kunduchi?

    28.Ikiwa Lipumba anaamini kwamba bila CUF hakiwezi kwenda kokote na tena akijiamisha kuwa ana wajibu wa kuendelea kuongoza chama ha CUF, haoni kuwa hiyo peke yake ni sababu ya kumfanya akataliwe kurudi? Kumbe amekuwa Mwenyekiti kwa miaka 20 na hakuwahi kutengeneza watu ambao wanaweza kuwa viongozi siku za mbeleni? Ikiwa huu ndiyo ulikuwa uenyekiti wake, wa kuzuia chama kuwa na viongozo mbadala, anaonaje akikaa kando ili chama cha CUF kijipange upya na kujitafutia mwisho mwema?

    29.Nilimsikia Lipumba akiongea kwenye mkutano alioandaliwa na wajiitao “wafia chama” uliofanyikia Mwananyamala. Kwanza alionekana kuponda viongozi waliopo Tanzania bara tangu ajiuzulu, alisema wameshindwa kuiongelea na kuipigania dhuluma waliyofanyiwa wazanzibari. Kimoyomoyo mimi nikajisemea, mbona wabunge wa CUF na CHADEMA na NCCR walipowasusa kina Magufuli na Shein kwa ajili ya kumshinikiza Magufuli achukue hatua – Ni Lipumba huyo huyo ndiye alikimbilia Ikulu wakati huo huo kumpongeza na kumuunga mkono Magufuli?

    30.Pili, nilimsikia Lipumba kwenye mikutano kadhaa na vyombo vya habari (baada ya kumuasi Magufuli), akianza kumponda sana rais huyo, tena akimtuhumu kwa kunyanyasa vyama vya upinzani na kudhibiti demokrasia. Nikajisemea kimoyomoyo, “yale ambayo Lipumba alienda kujifunza Rwanda wakati wa kampeni, akipelekwa kwa fedha za Serikali, si ndiyo hayo ambayo Magufuli amejifunza na sasa anatekeleza?”. Nikaendelea tena kujisemea moyoni “Si ni Lipumba huyu huyu ndiye alikuwa anamponda mgombea wa UKAWA Edward Lowassa mwaka jana na alijiuzulu kwenye chama cha CUF ili asihusike kumuunga mkono Lowassa? Kitendo chake kile si kilikuwa na maana kuwa hataki Lowassa ashinde? Kitendo hicho si kilikuwa pia kinamaanisha kuwa kama Lowassa hashindi basi lazima Magufuli angeshinda? Kwa hiyo, si Lipumba alikuwa anajua kuwa hatamuunga mkono Lowassa ili ashindwe na kwa hiyo Magufuli ashinde? Na kwa hiyo, kushinda kwa Magufuli si ndiko leo kumemfanya awe Rais wa Tanzania na ashindwe kabisa kushughulikia dhuluma ya Zanzibar na hata kuendeleza utawala wa kiimla huko nyumbani Tanzania? Kwa hiyo, kumbe Lowassa angesaidiwa na Lipumba kwenye kampeni mwaka jana na akashinda Urais wa Tanzania si ina maana Rais wa Jamhuri ya Muungano (Lowassa) angeelekeza tu mara moja kuwa Maalim Seif apewe ushindi wake Zanzibar?”.

    Nikaendelea kujisemea kimoyomoyo kuwa Usaliti wa Lipumba kwa UKAWA ndiyo ulichangia Lowassa asishinde na ndiyo ulichangia Magufuli ashinde. Sasa iweje leo hii, mtu aliyesababisha Dikteta aingie madarakani anapata ujasiri wa kusimama kulalamika kuwa Magufuli anaminya demokrasia? Si ni mwaka jana tu ndipo Lipumba aliona ni heri Magufuli wa CCM kuliko Lowassa wa UKAWA?
    Mambo haya 30 yamenifanya niendelee kutafakari ikiwa Lipumba ana washauri au La! Na ni kina nani? Nilimpigia simu mtu mmoja huko Tanzania, akanichekesha kuwa “washauri wa Lipumba ni kina Nditi” (Nditi ni kijana mmoja ambaye inasemekana hata darasa la saba hakufika na kila uchwao yeye hushinda Manzese vijiweni). Kijana huyo anasemekana kuwa kwa Lipumba kila uchwao na kumpa mikakati ya kisiasa kila siku tangu Mwenyekiti huyo ajiuzulu mwaka jana. Bado naendelea kuuliza na kuhoji, nani wanamshauri Lipumba? Wana nia gani na Alhaji huyu, mtu wa Mungu? Wanamtafuta nini kiongozi huyu Mstaafu wa CUF. Huku ughaibuni tunasubiri kusikia Mwisho wa Aibu ni nini.

    Abdallah Yusuph Juma, yabduljuma72@yahoo.com

    Hakuna maoni:

    Chapisha Maoni

    Search

    Chapisho Lililoangaziwa

    NEW HIT:OMMY DIMPOZ FT ALIKIBA-KAJIANDAE

    Toa Maoni yako

    Jina

    Barua pepe *

    Ujumbe *

    Wanaofuata

    Propellerads