Tunakupa unachohitaji sasa na baadae

Propellerads
  • WELCOME TO Adonisstunner Blog FOR UPDATED NEWS AND ENTERTAINMENTS

    Search

    Alhamisi, 1 Septemba 2016

    RAIS MAGUFULI ABADILI HISTORIA, JWTZ KUHAMIA DODOMA,, CHUO CHA ULINZI WA TAIFA KUANZISHWA,,,


    Kwa muda mrefu sasa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na makao yake jijini Dar es Salaam. Makao hayo yamekuwa yakihama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

    Jeshi hilo lililoundwa mwaka 1964 lilikuwa na makao yake zilipo ofisi za Kampuni ya Maji ya Dar es Salaam (Dawasco) kabla ya kuhamia Army House na baadaye katika makao makuu ya sasa ya Upanga, ambayo awali ilikuwa shule ya msingi ya madhehebu ya Aga Khan.

    Agosti 31, 2015, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa eneo la Makongo Juu, Kambi ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam.

    Akizundua ujenzi huo, Rais Kikwete alisema ndoto ya miaka mingi ya kuwapo kwa makao makuu ya ulinzi wa taifa sasa imetimia.

    “Namaliza wajibu wangu wa Amiri Jeshi Mkuu nikiwa mtu mwenye furaha sana kwa sababu ya jambo hili.”

    Hata hivyo, ndoto hiyo ya kuwa na makao makuu mapya ya JWTZ sasa imefutika baada ya Rais John Magufuli kuagiza makao makuu ya Serikali yawe mkoani Dodoma.

    Akihutubia muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni, Rais Magufuli alisema atahakikisha azma ya muda mrefu ya kuhamishia makao makuu ya Serikali mkoani Dodoma inatekelezwa katika awamu yake hii ya uongozi.

    Miongoni mwa taasisi zinazotakiwa kuhama ni JWTZ, hivyo hata yale makao makuu yaliyokuwa yakijengwa eneo la Lugalo sasa yanahamishwa.

    Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Ngemara Lubinga anasema tayari Jeshi hilo limeshaitikia wito huo kwa kuhamisha Makao yake Makuu yaliyokuwa yahamie Lugalo kutoka Upanga jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma.

    “Mpango ni kama alivyoagiza Rais, kwa maana kwamba tumeshachukua eneo letu kule. Kuna eneo ukipita Ihumwa ukitokea mjini kuna kijiji kinaitwa Mtumba na barabara imeshachimbwa,” anasema na kuongeza:

    “Kwa sasa ofisi bado haijajengwa, lakini kuna nyumba zilizojengwa na hazijahamiwa ndiyo tutazifanya kuwa ofisi za kuanzia,” anasema Kanali Lubinga.

    Hata hivyo, anasema kazi hiyo haitakuwa ya pamoja na wala bajeti yake hawezi kuiweka wazi.

    “Kwa sasa siwezi kusema bajeti ni kiasi gani si unajua kuwa bajeti ya Jeshi huwa haiwekwi wazi? Lakini kuhama tunahama,” anasema.

    “Si unajua kwamba tunataka kuhama Upanga na Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliweka jiwe la msingi pale Lugalo? Sasa tunahamisha na jiwe la msingi tunapeleka Dodoma,” anasema Kanali Lubinga.

    Ujenzi huo wa makao makuu ya jeshi ambao dhana yake ni ya siku nyingi ulitarajiwa kugharimu kiasi cha dola za Marekani 55 milioni na ungechukua miaka miwili kukamilika.

    Gharama hizo ni pamoja na zile za upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro, shughuli ambazo zilifanywa na Kampuni ya Norinco ya China pamoja na gharama za ujenzi.

    Makao Makuu hayo yangehusisha Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Makao Makuu ya Ngome (Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania - JWTZ) na Makao Makuu ya Kamandi za Nchi Kavu, Maji na Anga za JWTZ.

    Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange anasema ujenzi huo unaofanywa na kampuni ya Norinco ya China umetokana na misingi miwili mikuu ambayo ni urekebishwaji wa muundo wa JWTZ ambao umekuwa unafanyika tangu miaka ya 1980 na hali ya mazingira ya sasa ya eneo la Upanga ambako yako makao makuu ya Ngome.

    Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Ali Mwinyi alisema kuwa ujenzi wa makao makuu hayo ni mradi mwingine mkubwa ulioanzishwa na kutekelezwa katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.

    Alitaja miradi mingine mikubwa kuwa ni kujengwa na kuanzishwa kwa Chuo cha Ulinzi wa Taifa (The National Defence College), kujengwa na kuanzishwa kwa Chuo cha Ukamanda kilichoko Duluti, mkoani Arusha na ujenzi mkubwa wa nyumba 10,000 za kuishi wanajeshi katika mikoa mbali mbali.

    Jeshi la polisi tayari limeshaweka wazi mpango wake wa kuhamisha makao yake makuu Dodoma.

    Akizungumzia uamuzi huo, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Nsato Marijani anasema utekelezaji wake utaanzia kwa viongozi.

    “Agosti (mwezi uliopita) tunahamia Dodoma. Tutafanya hivyo kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri Mkuu,” anasema Marijani.

    Anaeleza jinsi mpango huo utakavyotekelezwa akisema Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na makamishna kadhaa watatakiwa kuhamia Dodoma huku wengine wakibaki kuendelea na majukumu yao Dar es Salaam. Hata hivyo hakusema makao makuu hayo yatakuwa wapo mkoani Dodoma.

    Wakati Taasisi ya Kupambana Kuondoa Rushwa (Takukuru) ikifurahia uboreshwaji wa ofisi zake likiwamo jengo lake jipya la makao makuu lililopo Upanga jijini Dar es Salaam, sasa nao watalazimika kwenda Dodoma.

    Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba anasema jitihada za kuhamia Dodoma zinaendelea na makao hayo makuu yatatumika kama ofisi za mikoa.

    “Sisi tuko mbioni kuhamia Dodoma wakati wowote. Hili jengo litatumika tu, tunazo ofisi za wilaya mbili tulizopanga, zitahamia hapa, kwa hiyo hakuna hasara yoyote,” anasema Misalaba.

    Anakiri kuwa uhamiaji huo utagharimu tena ujenzi wa ofisi mpya ya makao makuu mkoani Dodoma japo hakufafanua gharama watakayoingia.

    “Kwa sasa tuna kiwanja kule Dodoma, wewe subiri tu, kwa sasa hatusemi sana,” anasema Misalaba.

    Chanzo: Mwananchi

    Hakuna maoni:

    Chapisha Maoni

    Search

    Chapisho Lililoangaziwa

    NEW HIT:OMMY DIMPOZ FT ALIKIBA-KAJIANDAE

    Toa Maoni yako

    Jina

    Barua pepe *

    Ujumbe *

    Wanaofuata

    Propellerads